MATANGAZ0 YETU 



Breaking

Saturday, 3 February 2018

SERIKALI YAFUTA TOZO ZAIDI YA 80,ADA 139 KATIKA MAZAO YA KILIMO






Na. Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 imefuta ada na tozo zipatazo 80 kati ya tozo na ada 139 zilizokuwa zinatozwa katika mazao ya kilimo nchini ambazo zilibainika kutokuwa na tija kwa wakulima.Naibu Waziri wa Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa ameyasema hayo leo Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Nsimbo Mhe. Richard Philip Mbogo juu ya zao la tumbaku kuwa na tozo nyingi ambazo ni mzigo kwa wakulima."Kutokana na maamuzi hayo ya kufuta tozo hizo za mazao ya kilimo, kwenye tasnia ya tumbaku jumla ya tozo kumi (10) zilifutwa na tozo mbili (2) zilipunguzwa viwango," alifafanua Dkt. Mwanjelwa.Aidha amesema katika tozo ambazo zilitamkwa kufutwa katika tasnia ya tumbaku kwenye Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2017/2018 ni pamoja na mchango kwa Chama cha Ushirika cha Msingi kiasi cha USD 0.072 kwa kilo pamoja na mchango wa chama cha Ushirika cha Mkoa kiasi cha USD 0.030 kwa kilo.Hata hivyo amesema kuwa,  baada ya majadiliano ya wadau katika tasnia ya tumbaku, tozo hizo zilirejeshwa kutokana na umuhimu wake katika kuwezesha usimamizi unaofanywa na vyama vya ushirika katika tasnia hiyo.Vile vile ameyataja mazao mengine yaliyopunguziwa ada na kodi kuwa ni kahawa ambapo jumla ya tozo 17 zilifutwa na tozo moja (1)  ilipunguzwa kiwango. Kwa upande wa sukari, tozo 16 zilifutwa, tasnia ya pamba tozo  mbili (2) zilifutwa, tasnia ya mbegu tozo saba (7) zitafutwa na tasnia ya mbolea tozo (3) zilifutwa na tozo moja (1) ilipunguzwa kiwango.Dkt. Mwanjelwa amesema tozo 20 zilizokuwa zinatozwa na vyama vya ushirika katika ngazi mbalimbali nazo zilifutwa. Wakati huo huo Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Mhandisi Ramo Makani Mbunge wa Tunduru Kaskazini kuhusu mazao yaliongoza katika kuchangia pato la Taifa kwa miaka mitano alisema,  takwimu zinaonesha kuwa mchango wa mazao ya Kilimo, Misitu na Uvuvi katika Pato la Taifa  (GDP) kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita ulikuwa ni ni 31.1% mwaka 2012, 25.0% mwaka 2013, 24.5% mwaka 2014, 23.5% mwaka 2015 na 26.4% mwaka 2016.Dkt. Kijaji amesema mazao yaliyoongoza katika mauzo kwenye soko la nje na kuchangia kwa sehemu kubwa katika Pato la Taifa ni Tumbaku, Korosho, Kahawa, Pamba na Chai ambapo fedha za kigeni zilizotokana na mauzo ya mazao hayo ni Dola za Kimarekani milioni 793.4  mwaka 2015 na Dola za Kimarekani milioni 895.5 mwaka 2016.

No comments:

Post a Comment