Idadi ya waliofariki kutokana na moto wa misituni katika maeneo mawili ya jimbo la California, magharibi ya Marekani imeongezeka na kufika 31 na hivyo kufikia kiwango cha historia cha vifo kutokana na moto katika jimbo hilo.
Karibu watu robo milioni walilazimika kukimbia makazi yao na gavana wa jimbo akisema sababu moja ya moto huo mkali ni mabadiliko ya hali ya hewa.
Moto wa kihistoria
Moto uliosababisha maafa makubwa zaidi katika historia ya jimbo hilo la California ulianza kaskazini ya jimbo hilo na kuteketeza kabisa mji wa Paradise ambako watu 23 walipoteza maisha na wazimamoto wameripoti kuwa wamegundua maiti nyingine 6 Jumatatu. Zaidi ya watu 100 wanaoishi katika mji huo hawajulikani waliko.
Moto huo mkali uliopewa jina la Camp Fires unateketeza misitu ya sehemu za chini ya milima ya Sierra Nevada ambako karibu watu laki mbili na nusu wamekimbia makazi yao na zaidi ya nyumba na majengo 6400 kuteketezwa kabisa .
Gavana wa jimbo la California Jerry Brown anasema wako katika zama zisizo za kawaida za hali ya hewa.
Tamko la Gavana Jerry Brown
Hatujui sababu za moto huo. Mji wa Paradaise ulijitayarisha vya kutosha kukabiliana na hali mbaya ya hewa kutokana na ukame na kukauka kwa mimeya lakini upepo mkali umesababisha hali hii mbaya kutokea na inatubidi kufahamu mabadiliko haya kwani tunaishi katika mazingira yasiyo ya kawaida.
Gavana Brown amemuoba Rais Donald Trump kutangaza kuwa moto huu ni janga kuu ili kuongeza msaada wa dharura na kuwasaidia wakazi kupata fidia.
Rais Trump wiki iliyopita alikosowa usimamizi mbaya wa misitu ya California kuwa ni sababu ya moto ya mara kwa mara, lakini maafisa wa jimbo wanasema moto unatokea zaidi katika misitu inayosimamiwa na serikali kuu.
Miji ya matajiri hatarini
Na mamia ya maili kusini mwa jimbo hilo watu wawili wamepoteza maisha yao katika eneo la Woolsey na moto unatishia mji wa matajiri wa Malibu karibu ya Los angeles. Maafisa wa mji huo wanasema upepo mkavu unaovuma huko unatazamiwa kuendelea hadi kesho Jumanne na kuongeza ukali wa moto na hali ya dharura ya watu kuhama .
Timu za wazima moto wameweza kudhibiti asili mia 25 tu ya moto wa Camp Fires huko kaskazini mwa jimbo na asili mia 10 tu katika maeneo ya kusini.
Wakazi wapoteza kila kitu
Wakazi walioweza kurudi katika mji wa paradise kutizama hasara waliopata wanalia kwa masikitiko kupoteza kila kitu.
Tulilazimika kukimbia jana usiku hadi mji wa Topanga ilikutafuta maeneo ya usalama na nimerudi kutokana na habari kwamba kuna nyumba moja ilibnusurika. Na hivyo niko hapa kutizama jinsi majirani zetu walivyoppoteza mali yao.
Maafisa wa uwokzi na wazima moto wanasema hawana hakika lini wataweza kudhibiti mioto hiyo yote kwa hivi sasa.
No comments:
Post a Comment