MATANGAZ0 YETU 



Breaking

Tuesday, 4 December 2018

Ukaribu wa Rais Magufuli, Lowassa Waibua Minong'ono


Mjumbe wa Kamati ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Edward Lowasa ameonekana kutafsiriwa kwa sura mbili tofauti mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika kipindi cha siku 6.

Rais Magufuli na Lowasa wamekuwa wakikutana mara kwa mara na kutoleana sifa za kiutendaji jambo ambalo limeonekana kutokuwa la kawaida kutokana upinzani mkali uliokuwepo baina yao kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, lakini pia msimamo wa viongozi wengine wa upinzani nchini dhidi ya serikali ya Rais Magufuli.

Novemba 27 mwaka huu wakati Rais Magufuli, akifungua maktaba mpya ya chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) Rais Magufuli alimtolea sifa Waziri Mkuu huyo wa zamani kwa kujitokeza kushiriki kwenye matukio mengi kama hayo.

"Kwenye uchaguzi huwa kuna kushinda na kushindwa, mimi nakupongeza kwa moyo wa kweli na uzalendo kwa Tanzania, na mimi nasema kwa dhati tunahitaji watu waliokomaa kutoka kwenye vyama mbalimbali, kama wewe Mzee Lowassa , wewe ni 'Super man'," alisema Rais Magufuli.

"Maendeleo hayana chama, ndiyo maana Mzee Lowassa yupo hapa, nikushukuru kwa utulivu wako nilipokutupa chini baada ya uchaguzi ulikaa kimya, maana tuligombea mimi na wewe lakini wengine wanapiga kelele tu, kwakweli nikupongeze kwa uzalendo," aliongeza.

Tukio hilo lilikuwa ni la pili kwa Rais Magufuli kukutana na Mgombea huyo wa Urais mwaka 2015 kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambapo Januari mwaka huu viongozi hao walikutana Ikulu Jijini Dar es salaam, na Rais Magufuli alimpongeza Lowassa juu ya uvumilivu wake kwenye siasa.

Desemba 02 mwaka huu akiwa ziarani Jijini Arusha, Rais Magufuli alitaja sura ya pili ya Edward Lowassa baada ya kupokea malalamiko ya maji, kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Monduli, Julius Kalanga.

"Kalanga, Mbunge wa Monduli aliwahi kuniomba maji akiwa CHADEMA, lakini amesahau kuwa Lowassa amewahi kuwa Waziri wa Maji, simsemi mzee wangu namaanisha kuwa uzalendo unaanzia nyumbani, nikupongeze Kalanga kwa ujasiri wako wa kurudi huku, maji utapata," alisema Rais Magufuli.

Mbali na sura mbili za Lowassa kwa Rais Magufuli, lakini kiongozi huyo amekuwa akisifiwa mara kwa mara na baadhi ya viongozi wa serikali na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda na Katibu Mkuu CCM, Dkt Bashiru Ally kwa siasa zake.

No comments:

Post a Comment